The House of Favourite Newspapers

Jonesia Rukyaa Mambo 10 kuhusu refa wa Simba vs Yanga

0

Refa (2)

Refa Jonesia Rukyaa wa Kagera.

SIMBA na Yanga zinatarajiwa kukutana kesho Jumamosi katika Ligi Kuu Bara ambapo ni mchezo wa raundi ya pili baada ya ule wa awali Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, Septemba 26, 2015.

Mechi baina ya timu hizo huwa inakuwa na presha kubwa bila kujali michuano ambayo inazikutanisha timu hizo zenye upinzani wa jadi ambazo zote makao makuu yake ni Kariakoo jijini Dar es Salaam
Mwamuzi wa kati wa kesho atakuwa Jonesia Rukyaa wa Kagera, atasaidiana na Josephat Bulali (Tanga), Samwel Mpenzu (Arusha), mwamuzi wa akiba ni Elly Sasii (Dar) na kamisaa wa mchezo ni Khalid Bitebo (Mwanza).

Tunakuchambulia mambo kadhaa Jonesia mbaye kutajwa kwake katika mchezo huo kulisababisha gumzo hasa kuhusu kama ataweza kuumudu mchezo huo! Maswali hayo yanatokana presha ya mchezo huo hasa kipindi hiki ambacho Simba na Yanga zote zina nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo:

Alizaliwa mwaka 1988
Jonesia alizaliwa mwaka 1988 pia ni mwenyeji wa Mkoa wa Kagera.

Anaishi na bibi yake
Taarifa ambazo gazeti hili linazo ni kuwa Jonesia anaishi pamoja na bibi yake, wazazi wake wapo lakini haishi nao.

Ni mfanyabiashara
Nje na mchezo wa soka, binti huyo ni mfanyabiashara na biashara zake zipo Kagera.

Mtani Jembe pigo la kwanza
Mechi yake ya kwanza kubwa kuchezesha tangu alipoanza fani hiyo ilikuwa ni ya Mtani Jembe ya Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa iliyopigwa Desemba 13, 2014.
Yanga ilifungwa mabao 2-0, mchezo huo ulianza kwa presha kubwa na almanursa umshinde katika dakika za mwanzo lakini baadaye alitulia na kuumudu mpaka mwisho.

Jonesia & Bulali wanaendana
Katika mechi ya Mtani Jembe aliyochezesha, mmoja wa waamuzi wa pembeni alikuwa Josephat Bulali wa Tanga, huyu pia atakuwa naye kesho pia akiwa pembeni, inavyoonekana wahusika wameona wanaweza kufanya kazi pamoja.

Kigogo alimtishia maisha
Baada ya kuchezesha mechi ya Mtibwa Sugar dhidi ya Ruvu Shooting, mwaka jana, kigogo mmoja alimtishia maisha kwa madai ameinyonga timu yake. Gazeti hili lilionyeshwa SMS na jina la kigogo huyo, taarifa hizo zilifika TFF lakini suala hilo likapita kimyakimya.

Atishiwa tena
Baada ya kuchezesha mchezo wa Stand United dhidi ya Azam FC, mwamuzi huyo alitishiwa na kiongozi mmoja kwa madai ya kuipendelea timu moja kati ya hizo. Championi Ijumaa lilipewa jina la kiongozi huyo lakini hakukuwa na maelezo ya kina.

Rekodi ya mwamuzi mdogo
Alipochezesha mechi ya Nani Mtani Jembe aliweka rekodi ya kuwa mwamuzi wa kwanza wa kike kuchezesha mechi hiyo ya wapinzani pia kuwa mwamuzi mdogo zaidi kupewa beji ya Fifa nchini aliyoipata wiki kadhaa baadaye.
Tangu mwaka 2006, Tanzania imekuwa na waamuzi watatu wa kike wa kati waliopata beji ya Fifa ambao ni Flora Kashaija, Isabela Kapera wote wa Dar es Salaam na Judith Gamba wa Arusha.

Kocha Simba alimsifia
Katika hali ya kushangaza, wakati makocha wengi wamekuwa wakiwalalamikia waamuzi kila mechi, Kocha wa Jackson Mayanja akiwa anainoa Coastal Union, alisifia uwezo wa Jonesia pamoja na waamuzi wenzake mara baada ya mchezo dhidi ya Simba ambapo Coastal ilifungwa bao 1-0, Oktoba, 2015.
Katika mchezo huo, Jonesia alikuwa pamoja na John Kanyenye, Grace Wamara, mwamuzi wa akiba akiwa ni Omar Kambangwa. Kwa sasa Mayanja ni kocha wa Simba.

Bado yupoyupo
Miezi kadhaa iliyopita, gazeti hili liliwahi kumuuliza mwamuzi huyo juu ya maisha yake ya ndoa, alijibu kwa ufupi tu kuwa: “Sijaolewa.” Uchunguzi unaonyesha kuwa mpaka sasa bado hajaingia katika ulimwengu huo wa wapendanao.

Leave A Reply