Na: Alfred Lukonge.
Maofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu nchini TFS wamefanya ziara katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA ikiwa na lengo la kujifunza uchakataji wa bidhaa za mianzi pamoja na uzalishaji bora wa miche ya zao hilo.
Akizungumza katika ziara hiyo Bw. Paulo John Lyimo kutoka Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii SUA amesema kuwa mmea wa muanzi hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali kama vile viti na vitanda, hivyo watu wakitumia teknolojia hiyo itasaidia kupunguza uharibifu wa misitu.
Bw. Lyimo amebainisha kuwa mianzi ni rasilimali zenye manufaa makubwa tofauti na wengi wanavyodhani na kuwataka watanzania kutumia mimea hiyo katika shughuli zao za kuzalisha kipato.
Kwa upande wake Mkuu wa msafara kutoka TFS ambaye pia Meneja wa Shamba la Miti Ruvu Kaskazini Bi. Fortunate Senya amesema kuwa ziara hiyo imewapa hamasa kuanza kuchakata bidhaa za mianzi pamoja na kutoa ahadi ya kuwaelimisha watanzania matumizi sahihi ya mmea huo.
Aidha amewataka watanzania kupanda mianzi kwa kuwa ukuaji wake huchukua miaka michache ili iwe mbadala wa mazao ya misitu kama vile mbao ambazo upatikanaji wake huathiri misitu.
Naye Bw. Ezra Richard Chomola Msaidizi wa Meneja wa Shamba la Miti Ruvu Kaskazini, akitoa neno katika ziara hiyo amesema kuwa shamba lao la mianzi bado ni changa hivyo wanapita sehemu mbalimbali kujifunza wenzao wanafanyaje ili kuboresha shamba lao.
Amesema kuwa lengo la Wakala wa Misitu Tanzania ni kuanzisha mashamba mapya ya miti ili ipandwe kwa wingi kwenye maeneo yaliyoathirika maana ni malighafi nzuri katika utengenezaji wa samani za ndani.